Waziri wa Uchukuzi, Dk. Harrison Mwakyembe
Waziri
wa Uchukuzi, Dk. Harrison Mwakyembe, ameipa miezi mitatu menejimenti ya
Shirika la Reli la Tanzania na Zambia (Tazara), kuwalipa wafanyakazi
malimbikizo ya mishahara zaidi ya Sh. milioni 624.4 kwa wakati na
wakishindwa waache kazi.
Alitoa agizo hilo jana wakati akizungumza na wafanyakazi wa Tazara Mbeya
ambao walimlalamikia kuwa tangu Mei hadi sasa hawajalipwa mishahara
hali inayowafanya wakabiliwe na hali ngumu ya maisha.
Alisema miezi mitatu ikipita kama menejimenti itakuwa haijabadilika,
Naibu Mkurugenzi Mkuu wa Shirika na Mkurugenzi wa Mkoa wa Mbeya waandike
barua ya kuacha kazi mara moja kabla hajawafukuza yeye.
Dk. Mwakyembe alisema serikali imeunda timu ya wataalam ambao ni
wanasheria kutoka Tanzania na Zambia ambao watapitia upya mkataba wa
Tazara kutokana na shirika kukabiliwa na matatizo mengi ambayo
yanatokana na kuendeshwa kwa ushirikiano wa nchi mbili.
“Nimechoshwa na menejimenti ya Tazara, wanashindwa kulipa mishahara ya
wafanyakazi halafu wanaendelea kuwapo, mna mabilioni ya fedha mnawadai
watu halafu mnashindwa kukusanya,” alisema Dk. Mwakyembe.
Awali, Mwenyekiti wa Chama cha Wafanyakazi wa Reli Tanzania kanda ya
Mbeya (Trawu), Christopher Kaziyo, alimweleza waziri kuwa wafanyakazi
wanashangaa kutolipwa mishahara kwa miezi mitatu wakati kila mwezi
kumekuwa na ongezeko la mizigo inayosafirishwa na Tazara.
Kaziyo alisema katika kipindi cha kuanzia Mei hadi Julai mwaka huu
mizigo iliyosafirishwa ni tani 80,922 na kiasi cha zaidi ya Sh. bilioni
tisa zimelipwa na watu waliosafirishiwa mizigo hiyo. Alisema wafanyakazi
pia wanalalamika michango yao ya NSSF kutopelekwa benki kwa zaidi ya
miaka 10 jambo ambalo linazua maswali mengi wafanyakazi hao
watakapostaafu.
CHANZO MASAMA BLOG.
0 comments:
Chapisha Maoni