Searching...
Jumamosi, 8 Februari 2014

MASIKINI MOYES,JINAMIZI BAYA LINAENDELEA KUMUANDAMA,NYOTA WAKE KUTIMKA MWISHONI MWA MSIMU HUU.

Nemanja Vidic
NEMANJA VIDIC.
Nemanja, beki mwenye nguvu, shupavu, shujaa na kiongozi uwanjani, amebwaga manyanga baada ya miaka minane ya kukipiga Old Trafford na amekiri kwamba ataondoka mwishoni mwa msimu huu.

Mbabe huyo wa kimataifa wa Serbia ameichezea Manchester United tangu mwaka 2006, lakini hataendelea kuwapo tena klabuni hapo mara baada ya msimu huu mkataba wake utakapomalizika rasmi.

“Sifikirii kubaki England kwa sababu klabu pekee ambayo nilitaka kuichezea hapa ni Manchester United. Sikuwahi kufikiria kama ningetwaa mataji 15. Hata hivyo nimeamua kuondoka mwishoni mwa msimu. Nataka kujipa changamoto mpya,” alisema Nemanja katika taarifa rasmi aliyoituma katika mtandao wa klabu yake.

Vidic, ambaye uhamisho wake wa Pauni 7 milioni kutoka Spartak Moscow kwenda Old Trafford ulitangazwa siku ya Krismasi ya mwaka 2005, alikuwa nahodha wa Manchester United wakati ilipotwaa taji la 20 la Ligi Kuu England kihistoria msimu uliopita chini ya kocha Alex Ferguson.

“Nimekuwa na miaka minane ya kushangaza sana hapa. Muda wangu katika klabu hii kubwa siku zote utazungumzwa kama muda bora wa maisha yangu ya soka,” aliongeza.

“Sitausahau usiku ule mzuri Moscow (wakati Man United ikiichapa Chelsea na kutwaa ubingwa wa Ulaya mwaka 2008), ni kumbukumbu nitakazoishi nazo kwa miaka yote nitakayoishi hapa duniani.”

Vidic aliichezea Manchester United kwa mara ya kwanza Januari 25, 2006 katika pambano la Ligi Kuu England dhidi ya Blackburn Rovers na kuanzia hapo alitwaa mataji matano ya ligi hiyo, moja la Ligi ya Mabingwa Ulaya na matatu ya Kombe la Ligi.

Inadaiwa kwamba tayari beki huyo ana makubaliano ya kujiunga na Galatasaray ya Uturuki kwa mshahara mnono huku akitarajiwa kujiunga na wakali wengine waliowahi kukipiga Ligi Kuu England kama vile Didier Drogba na Emmanuel Eboue.

Itakumbukwa kuwa uhusiano wake wa muda mrefu wa uwanjani na beki mwingine wa United, Rio Ferdinand, ambaye pia anatarajiwa kutangaza kutundika daruga muda wowote kuanzia sasa.
 Hii ni moja ya picha zilizotumwa kwenye mitandao ya kijamii na wapenzi wa klabu ya Manchester United wakimnanga kocha wao Moyes kwamba anawaacha makamanda wake Nemanja Vidic na Van persie kutimka huku jahazi la klabu hiyo likizama.

0 comments:

Chapisha Maoni

 
Back to top!