Ruvuma/Songea/Tanga. Katibu
Mkuu wa Chadema, Dk Willibrod Slaa amesema kuwa chama hicho kitachukua
uamuzi mgumu ikiwa wabunge wa CCM watajikita katika kulinda masilahi yao
kwenye Bunge Maalumu la Katiba kinyume na maoni ya wananchi.
Akiongozana na Mbunge wa Iringa Mjini, Mchungaji Peter Msigwa, Dk Slaa
aliwaonya wabunge wa CCM kutotumia wingi wao bungeni kutetea masilahi ya
chama chao. “Kamwe wasithubutu kwani Chadema itachukua uamuzi mgumu
ambao kwa sasa si vizuri kuutaja,” alisema Slaa.
Alionya akisema ni lazima wabunge watoe maoni ambayo yana masilahi ya wananchi wote na siyo vyama.
Katika hatua nyingine, alisema Chadema itasusia kura ya maoni iwapo
daftari la wapiga kura halitaboreshwa kwa ajili ya mchakato wa Katiba.
Alisema kwa sasa chama hicho kinasambaza fomu maalumu nchi nzima kwa
ajili ya watu wasio na vitambulisho vya kupiga kura wajiorodheshe.
“Kuna maelfu ya watu waliopoteza vitambulisho vyao vya kupigia kura na
wengine wamefikia umri wa kupiga kura lakini Serikali haioni suala hilo
kuwa ni muhimu,” alisema.
Alisema uchunguzi wa chama hicho umebaini watu zaidi ya 5,000,000 hawana
vitambulisho vya kupigia kura japokuwa tayari wamefikia umri wa kupiga
kura.
Ili kuhakikisha Bunge la Katiba linakuwa na manufaa, Dk Slaa aliwataka
wananchi kufuatilia mjadala juu ya Katiba Mpya kwa makini ili kuwabaini
wabunge wasioitakia nchi hii mema.
Alisema wabunge wa namna hiyo wamepanga kutengeneza Katiba ya viongozi badala ya katiba ya wananchi.
Baadaye katika mkutano uliofanyika katika Uwanja wa Matarawe mjini
Songea mvua kubwa ilinyesha, lakini wananchi waliofurika hawakujali
kunyeshewa badala yake walionyesha shauku ya kuendelea kumsikiliza Dk
Slaa.
0 comments:
Chapisha Maoni