Searching...
Jumanne, 21 Januari 2014

KIMBUNGA KIKALI CHAIKUMBA MBALIZI MBEYA,WATU WENGI WAJERUHIWA,NYUMBA ZAEZULIWA

Wananchi wa Mji mdogo wa Mbalizi Wilaya ya Mbeya nje kidogo ya Jiji la Mbeya walijikuta katika wakati mgumu baada ya kupata matukio mawili makubwa kwa wakati mmoja huku watu kadhaa wakihofiwa kujeruhiwa na kukimbizwa katika Hospitali Teule ya Ifisi kwa ajili ya Matibabu.

Tukio la kwanza kuwakumba wakazi hao ni kumbunga kilichoambatana na upepo mkali ambacho kiliezua nyumba zaidi ya 30  yakiwemo Makanisa na kujeruhi watu ambao idadi yao haijafahamika maramoja ambao walikimbizwa Hospitali na kutibiwa.
Kwa mujibu wa mashuhuda wa tukio hilo walisema Kimbunga hicho kilianza majira  ya saa Sita Mchana leo kikivikumba vitongoji vya Iwindi, Jeshini, Mtakuja na Tarafani ambapo kimbunga hicho kiliezua mapaa ya nyumba za kuishi, maduka pamoja na makanisa.
Hata hivyo tathimini ya hasara iliyotokea bado haijajulikana ikiwa ni pamoja na idadi ya majeruhi na hali yao kutokana na wasemaji wa matukio hayo kutopatikana kwa wakati.
Hata hivyo katika tukio lingine lililotokea katika Stendi ya zamani Mbalizi ambapo kwa sasa ni kituo cha magari madogo yanayosubiri kukodiwa, walijikuta katika wakati mgumu baada ya kutokea kwa ajali mbaya iliyohusisha magari 9 na kujeruhi watu waliokuwemo.
Mashuhuda wa ajali hiyo wamesema chanzo cha ajali hiyo iliyotokea majira ya Saa Nane mchana ni gari aina ya Canter yenye namba za usajili T 186 AMM ambalo lilikatisha barabara bila kuangalia tahadhali likiwa linatokea barabara ya Utengule na kuvuka barabara ya TanZam likielekea barabara ya Kituo cha Polisi.
Walisema baada ya gari hiyo kuingia barabarani ilikutana na Roli kubwa lenye namba za usajili T 731 BLM likiwa na Trela lenye namba  T 126 BKS ambalo katika harakati ya kulikwepa lilipoteza mwelekeo na kuyagonga magari mengine ambayo yalikuwa yameegeshwa.

0 comments:

Chapisha Maoni

 
Back to top!