Mbunge wa Kigoma
Kaskazini, Zitto Kabwe amesema tuhuma alizosomewa na uongozi wa Chadema
katika kikao cha Kamati Kuu sizo zilizoelezwa na chama hicho mbele ya
waandishi wa habari na viongozi wa chama hicho.
Aidha, amesema kuwa vita
aliyopo siyo kati ya Chadema na Zitto, bali ni vita ya watu wengi,
akitaja magenge ya watu wanaotaka urais 2015 na walioficha fedha nje ya
nchi walioungana wakiona tatizo lao ni yeye hivyo kutaka kumwondoa
bungeni.
Akizungumza katika
mahojiano maalumu na gazeti hili kwa njia ya simu, Zitto alisema kuwa
hadi sasa bado hajapokea tuhuma 11 anazokabiliwa nazo, hivyo hajui
makosa hayo na bado anasubiri akabidhiwe kwa maandishi.
Ana ugomvi gani na viongozi wenzake?
Alipotakiwa kueleza
iwapo ana ugomvi na watu ndani ya Chadema, Zitto alisema kuwa huenda
mambo hayo yanatokea kwa sababu mahasimu wake wa kisiasa wa ndani na nje
wameamua kuungana na kupambana naye ili kumdhoofisha kisiasa kwa
masilahi yao.
“Matatizo yaliyopo ni
mafanikio yangu, …. nadhani hii siyo vita kati ya Chadema na Zitto, bali
ni vita ya watu wengi, pengine magenge ya watu wanaotaka urais na wale
walioficha fedha zao nje wamekaa pamoja wanaona tatizo lao ni Zitto…
wanajua siwezi kusemea nje maana sina kinga…, hivyo wanataka kuniondoa
bungeni…” alisema.
Aliongeza kuwa kwenye
siasa kinachohitajika ni kusimamia misingi, jambo alilosema binafsi
amekuwa akilifanya katika kipindi chake chote cha kisiasa.
Zitto alisema kuwa ni
vyema wananchi wakawapima wabunge wao kwa kazi wanazozifanya bungeni
akibainisha kuwa kati ya mwaka 2011 hadi 2013, yeye amewasilisha hoja
nyingi nzuri zilizo na mashiko ikilinganishwa na wabunge wenzake
wanaomtuhumu kutumiwa na CCM.
“Je, mbunge anayetumika
na Chama Cha Mapinduzi anaweza kupeleka hoja ya kumng’oa Waziri Mkuu na
kumshinikiza Rais mpaka akasimamisha kazi mawaziri wanane? Je, mbunge
anayetumika anaweza kushikia bango watu wanaotorosha fedha nje ya nchi?”
alihoji Zitto.
0 comments:
Chapisha Maoni