Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete akizungumza na Waziri wa Uchumi, Biashara na Viwanda wa Japan, Mheshimiwa Toshimistu Motegi alipokutana na kufanya mazungumzo naye  Ikulu, Dar Es Salaam, leo Agosti 10, 2013

        Sasa Tanzania kuwa nchi lengwa ya Japan
·   Japan itasaidia Tanzania kuwa kitovu cha uwekezaji katika Afrika
· Kushiriki maboresho Reli ya Kati
· Kusaidia kupanua na kuboresha Bandari ya Dar Es Salaam
· Viwanda vya Japan kujengwa nchini kikiwemo cha kutengeneza pikipiki za Honda
· Ni matokeo ya Ziara ya Rais Kikwete Japan
JAPAN imeamua kuanzisha ushirikiano mkubwa zaidi na Tanzania ambako nchi hiyo itaifanya Tanzania kuwa nchi lengwa ya Japan na kuiwezesha kuwa kitovu cha biashara na uwekezaji katika Afrika kwa nia ya kuiwezesha kuwa na uchumi ulioimarika na wenye kuzalisha ajira nyingi kwa wananchi.
Uamuzi huo wa Japan ni matunda ya mazungumzo kati ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete na Waziri Mkuu wa Japan, Mheshimiwa Shinzo Abe yaliyofanyika Tokyo, Japan wakati Rais Kikwete alipotembelea nchi hiyo Juni, mwaka huu, 2013.
Uamuzi na msimamo mpya wa Japan umetangazwa rasmi leo, Jumamosi, Agosti 10, 2013 na Waziri wa Uchumi, Biashara na Viwanda wa nchi hiyo, Mheshimiwa Toshimistu Motegi alipokutana na kufanya mazungumzo na Rais Kikwete, Ikulu, Dar Es Salaam.
Kwa upande wa Tanzania, mazungumzo hayo yamehudhuriwa pia na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu anashughulika na Uwekezaji na Uwezeshaji  Mheshimiwa Mary Nagu, Waziri wa Viwanda na Biashara Mheshimiwa Dkt. Abdallah Kigoda na Waziri wa Uchukuzi Mheshimiwa Dkt. Harrison Mwakyembe.
Waziri Motegi amemwambia Rais Kikwete kuwa ametumwa na Waziri Mkuu Abe kufuatilia mazungumzo kati yao na kutangaza rasmi kuwa Japan imeiteua Tanzania kuwa nchi lengwa na kitovu cha uwekezaji wa Japan katika Afrika Mashariki na katika Afrika kwa jumla.
Waziri Motegi pia amemwambia Rais Kikwete kuwa pia amekuja Tanzania kutoa taarifa kuwa Japan iko tayari kushiriki katika kuboresha na kuifanya ya kisasa zaidi Reli ya Kati kwa kujenga njia ya kimataifa badala ya njia nyembamba ya sasa. Amesema kuwa Japan itatuma wataalam wake kuangalia jinsi gani ya kuanza kazi hiyo ya uboreshaji wa Reli hiyo.
Aidha, Mheshimiwa Motegi ametangaza kuwa Japan itashiriki katika upanuzi na uboreshaji wa Bandari ya Dar Es Salaam kwa kuifanya ya kisasa zaidi.
Waziri Motegi amesema kuwa katika azma ya Japan ya kuifanya Tanzania nchi ya mfano katika Afrika katika uwekezaji na uchumi ulioimarisha, amekuja na kundi la wafanya biashara wa Japan ambao wanaendelea kufanya mazungumzo na wafanyabiashara wa Tanzania kuona jinsi gani wanavyoweza kusaidiana katika kuwekeza katika uchumi wa Tanzania.
                        Waziri pia amesema kuwa moja ya malengo ya uamuzi huo wa Japan ni kuhakikisha kuwa bidhaa ambazo kwa sasa zinanunuliwa moja kwa moja kutoka Japan zitazalishwa hapa nchini katika viwanda ambavyo vitajengwa na makampuni ya Japan.
Kwa kuanzia amesema kuwa makampuni mawili ya Honda na Panasonic yamekubali kujenga viwanda nchini kimoja kwa ajili ya kutengeneza pikipiki za Honda hapa hapa nchini na kingine kwa ajili ya kutengeneza vifaa vya umeme.
“Huu ni mwanzo tu Mheshimiwa Rais kwa sababu kama nilivyosema kuwa tunataka Tanzania kuwa nchi mfano ya uwekezaji wa Japan  katika eneo hili la dunia na namna hiyo kwa pamoja tutakuwa tumeshirikiana katika kuongeza ajira kwa wananchi wa Tanzania,” Mheshimiwa Motegi amemwambia Rais Kikwete.
Waziri huyo pia amesema kuwa baadhi ya makampuni ya Japan yana mipango ya kuwekeza katika kilimo, na hasa kilimo cha pamba, na kuanzisha viwanda vya nguo hapa hapa nchini.
Wakati wa mazungumzo yao mjini Tokyo, Rais Kikwete alimtaka Waziri Mkuu Abe kuwekeza zaidi katika Afrika akisisitiza kuwa Japan ni moja ya mataifa makubwa duniani ambayo yamefanikiwa kupata soko kubwa katika Afrika na hasa soko la magari.
Uamuzi huo wa Japan na ziara ya Mheshimiwa Motegi inakuja wiki na miezi michache baada ya Tanzania kuwa imepokea viongozi wa mataifa mengi yakiwemo mataifa makubwa ya Marekani na China na inathibitisha ni kiasi gani siasa na sera za Tanzania zinavyokubalika duniani.