Mapigano hayo katika mji wa bandari Kusini mwa Somalia yamesabisha watu
wengi kuyahama makaazi yao na kuendelea kusababisha athari kubwa kwa
wananchi na kukwamisha juhudi za utoaji wa misaada ya kibinaadamu katika
eneo hilo.
Wahanga wengi wa mapigano hayo wamepata majeraha ya kuvunjika mifupa,
vichwa na vifua ambapo kwa mujibu wa WHO karibu majeruhi 40 walilazimika
kufanyiwa upasuaji.
Mji wa Kismayo kwa sasa ni uwanja wa mapambano kati ya wanamgambo
wanaohasimiana wakipigania udhibiti wa mji huo muhimu kimkakati.
Serikali ya kuu ya Somalia kwa sasa inavinyoshea kidole cha lawama
vikosi vya serikali ya Kenya ambavyo vimeweka kambi katika mji wa
Kismayo kwa kuwasaidia wanamgambo wa kundi moja dhidi ya wengine na
kuutaka umoja wa Afrika kutuma kikosi katika mji huo ambacho
hakitaegemea upande wowote.
Serikali ya Somalia imelalamika kwa umoja wa Afrika kuwa mwenendo wa
vikosi vya Kenya katika mji wa Kismayo vinahujumu juhudi za kijeshi za
kupambanana na wapiganaji wa kiislamu wa kundi la al-Shabab.
Mbali na hilo vikosi vya Kenya vinashutumiwa kwa kuwasaidia wapiganaji
wa kundi la Raskamboni Brigade, ambao walilisaidia jeshi hilo kuwafukuza
wapiganji wa Al-shabab nje ya mji wa Kismayo.
Kundi hilo linaloongozwa na Ahmed Madobe, kiongozi mwenye ushawishi
mkubwa katika maeneo yanayouzunguka mji wa Kismayo lakini asiyeungwa
mkono na serikali kuu ya mjini Mogadishu. Jeshi hilo la Madobe
linapigana na kundi lililokuwa likiongozwa na mbabe wa zamani wa kivita,
Barre Hirale.
Mapema wiki hii wizara ya mambo ya nje ya Somalia iliuandikia barua
Umoja wa Afrika kulalamika juu ya wanajeshi wa Kenya kuwa wamevuruga
mipango ya kuwa na kikosi cha pamoja mjini humo kinachoongozwa na
kamanda wa Somalia. Barua hiyo ilisema hatua hiyo imesababisha kuwepo
kwa makundi mbalimbali ya kiukoo na hivyo kuzorotesha amani na usalama
katika eneo la Jubba.
Mji wa Kismayo ni muhimu sana kwa serikali ya Kenya ambayo inataka
ukanda wa kirafiki karibu na mpaka wake na Somalia, ikiwa ni moja ya
sababu kuu za Kenya kutuma vikosi vyake kwenda Somalia kupambana na
wanamgambo wa A-shabab mwaka 2011.
Lakini makundi ya waasi yanayopigana katika mji wa Kismayo yameoneka
kuwa na hamu kubwa na injini ya mji huo wa Kismayo. Bandari ya mji hio
huingiza pato kubwa la kutegemea na imetumiwa kusafirishia mkaa katika
nchi za nje, bidhaa ambayo ilipigwa marufuku na Umoja wa Mataifa.
Mwandishi: Hashim Gulana/ APE
Mhariri: Josephat Charo
0 comments:
Chapisha Maoni