RAIS Jakaya Mrisho Kikwete amefanya mazungumzo kwa
njia ya simu na Rais wa Sudan Omar Bashir kufuatia kuuawa na kujeruhiwa
kwa askari wa Tanzania, walioko katika ulinzi wa kimataifa wa amani
katika jimbo la Darfur na kumtaka Rais Bashir kuchukua hatua za haraka
kuwasaka na kuwakamata waliohusika na kitendo hicho kiovu na kuwafikisha
mbele ya sheria haraka iwezekanavyo. Katika mazungumzo yao, Rais Omar
Bashir amekubaliana na Rais Kikwete na kumuahidi kuwasaka hadi
kuwakamata wale wote waliohusika na kuwachukulia hatua za kisheria.
Rais Bashir amemueleza Rais Kikwete kuwa binafsi anaamini kuwa
waliohusika ni wahalifu na hivyo kuahidi kuwa lazima watasakwa hadi
kukamatwa kwa ajili ya kuchukuliwa hatua. Rais Bashir amempa pole Rais
Kikwete kwa tukio hilo la kusikitisha ambapo wanajeshi wa Tanzania
wameenda nchini Sudan kulinda Amani na Usalama wa wananchi wa Sudan.
Mapema Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa(UN) Bw. Ban Ki Moon alimpigia
Rais Kikwete na kumpa pole kwa mkasa huo mkubwa na wa kusikitisha ambao
umewatokea wa Tanzania hao wakati wakiwa katika kutekeleza jukumu lao la
kulinda amani nchini Sudan.
Hadi sasa hakuna kikundi chochote ambacho kimekiri kuhusika na
shambulio hilo ingawaje kumekua na kutupiana lawama baina ya vikundi
vya kiserikali na vya waasi katika jimbo la Darfur. Mapigano baina ya
vikundi vya kikabila na koo mbalimbali zimesababisha mapigano na
uvunjifu mkubwa wa amani na usalama katika jimbo la Darfur kwa muda wa
miaka 10 sasa, na mara nyingi mapigano na tofauti zao hizo
zimesababisha vifo na uvunjifu wa amani kwa wananchi wa Sudan na wageni
pia.
Mwishoni mwa mwaka jana Wanajeshi wanne kutoka Nigeria waliuawa
karibu na El Geneina , Magharibi mwa Darfur ambapo pia inaelezwa na
Umoja wa Mataifa kuwa wanajeshi wapatao 50 wameuawa tangu kikosi hiki
cha Umoja wa Afrika kinachoundwa kwa pamoja chini ya Umoja wa Mataifa
(UNAMID) kianze operesheni yake mwishoni mwa mwaka 2007.
Taarifa za Umoja wa Mataifa pia zinaeleza kuwa kabla ya mashambulizi
yaliyofanyika dhidi ya kikosi cha Tanzania jumamosi iliyopita, wanajeshi
6 wanaolinda Amani wameuawa tangu oktoba mwaka huu ambapo pia
inasadikiwa kuwa watu wapatao 300,000 wameyakimbia makazi yao.
Hata hivyo kiini cha mgogoro huo unaosadikiwa kuwa ni ugomvi wa ardhi
na rasilimali zilizoko katika jimbo hilo nchini Sudan. Miili ya
maaskari hao saba wa Tanzania inatarajiwa kuwasili nchini ijumaa tarehe
19, Julai kwa ajili ya maziko.
0 comments:
Chapisha Maoni