Searching...
Jumatatu, 22 Julai 2013

LIGI KUU YA VODACOM 2013/2014 KUANZA AGOSTI 24,TAIFA STARS KWENDA KAMPALA J5

 
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Julai 22, 2013
Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) kuwania ubingwa wa Tanzania Bara msimu wa 2013/2014 inaanza kutimua vumbi Agosti 24 mwaka huu kwa timu zote 14 kuwa viwanjani katika miji saba tofauti.
Hata hivyo, kabla ya ligi hiyo kuanza kutakuwa na mechi ya kufungua msimu (Ngao ya Jamii- Community Shield) kati ya bingwa mtetezi Yanga na Makamu bingwa Azam itakayochezwa
Agosti 17 mwaka huu Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Mechi za VPL za Agosti 14 mwaka huu zitakuwa kati ya Yanga na Ashanti United (Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam), Mtibwa Sugar na Azam (Uwanja wa Manungu, Morogoro), na JKT Oljoro na Coastal Union (Uwanja wa Kumbukumbu ya Sheikh Kaluta Amri Abeid, Arusha).
Nyingine ni Mgambo Shooting na JKT Ruvu (Uwanja wa Mkwakwani, Tanga), Rhino Rangers na Simba (Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi, Tabora), Mbeya City na Kagera Sugar (Uwanja wa Kumbukumbu ya Sokoine, Mbeya), na Ruvu Shooting na Tanzania Prisons (Uwanja wa Mabatini, Mlandizi, Pwani).
Mzunguko wa kwanza wa ligi hiyo utamalizika Novemba 3 mwaka huu wakati wa pili utamalizika Aprili 27 mwakani.Ratiba ya mzunguko wa kwanza na wa pili imeambatanishwa.
TAIFA STARS KWENDA KAMPALA J5
Timu ya Taifa ya Tanzania (Taifa Stars) inaondoka Mwanza keshokutwa (Julai 24 mwaka huu) kwenda Kampala, Uganda kwa ajili ya mechi ya marudiano ya Kombe la CHAN itakayochezwa Jumamosi (Julai 27 mwaka huu) Uwanja wa Mandela kuanzia saa 10 kamili jioni.
Taifa Stars inayodhaminiwa na Kilimanjaro Premium Lager iko kambini jijini Mwanza chini ya Kocha Kim Poulsen tangu Julai 14 mwaka huu kujiandaa kwa mechi hiyo itakayoamua ni timu ipi kati ya hizo mbili itacheza Fainali za CHAN zitakazofanyika mwakani nchini Afrika Kusini.
Timu hiyo itaondoka Uwanja wa Ndege wa Mwanza saa 7.25 mchana kwa ndege ya PrecisionAir, na inatarajiwa kutua Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Entebbe saa 10.15 jioni.
Wakati huo huo, Kocha Kim Poulsen kesho (Julai 23 mwaka huu) atakuwa na mkutano na waandishi wa habari kuzungumzia maandalizi ya kikosi chake. Mkutano huo utafanyika saa 5 kamili asubuhi kwenye hoteli ya La Kairo jijini Mwanza.

Boniface Wambura
Ofisa Habari
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF)

0 comments:

Chapisha Maoni

 
Back to top!