Scholastica Wanjiru Githinji
Bi Scholastica Wanjiru Githinji akiwa kortini Nairobi Julai 12, 2013 ambapo alishtakwia kwa kosa la kupanga njama ya kumuua mumewe. Picha/PAUL WAWERU  
 
Na RICHARD MUNGUTI
KESHIA katika kampuni ya Kenya Power Ijumaa alishtakiwa kwa kupanga njama ya kumuua mumewe.
Bi Scholastica Wanjiru Githinji, 32, alifikishwa mbele ya Hakimu Mwandamizi Bi Elena Nderitu na kukana akishirikiana na watu wengine ambao hawajafikishwa kortini alipanga njama ya kumuua mumewe Bw Peter Mathenge Mukara.
Alishtakiwa alipanga njama hiyo na wauaji mnamo Juni 12, 2013 katika mtaa wa Buruburu kaunti ya Nairobi.
Bi Githinji aliyefunga ndoa na Bw Mukara 2010 na kumlipia mahari aliomba aachiliwe kwa dhamana.
Kupitia kwa wakili John Swaka, mshukiwa huyo alimsihi hakimu “asimsukumie kiwango cha juu cha dhamana.”
“Naomba korti imwachilie mshtakiwa kwa dhamana isiyo ya juu. Hii korti inapasa kuchukulia kwamba mshtakiwa hana hatia hadi ithibitishwe kwamba alipanga njama ya kumuua mumewe,”akasema Bw Sakwa.
Pia wakili huyo aliomba hakimu aamuru upande wa mashtaka “umkabidhi nakala za mashahidi ndipo aandae ushahidi mshukiwa atakaotoa pamoja na kuwahoji mashahidi.”
Kiongozi wa mashtaka Inspekta Mkuu Kinoti Marete hakupinga ombi hilo la Bi Githinji la kuachiliwa kwa dhamana.
“Sijapata maagizo yoyote nipinge mshtakiwa akiachiliwa kwa dhamana,”akasema  Insp Marete.
 Akitoa uamuzi wa ombi la dhamana, Bi Nderitu alimwamuru mshtakiwa alipe dhamana ya pesa tasilimu Sh500,000 ndipo aachiliwe afanye kesi akiwa nje.
“Ikiwa utashindwa kupata Sh500,000 utawasilisha mdhamini wa Sh1milioni,”akasema Bi Nderitu.
Hakimu pia aliamuru upande wa mashtaka umkabidhi mshtakiwa nakala zote Za mashahidi atayarishe ushahidi wake.
Kesi hiyo iliorodheshwa kusikizwa Agosti 30 mwaka huu.
Mshtakiwa aliamriwa afike kortini tena Julai 26 wakati wa kutajwa kwa kesi hiyo.
Upande wa mashtaka utawaita mashahidi zaidi ya watano miongoni mwao Bw Mukara ambaye pia ni mfanyakazi wa Kenya Power.
Bi Githinji alikamatwa Juni 11, 2013 na kuzuiliwa katika kituo cha polisi cha Kilimani hadi Ijumaa asubuhi alipotolewa akipelekwa katika Mahakama ya Milimani Nairobi.
Ndoa ya Scholastica na Bw Mukara haijabarikiwa na mtoto.
Keshia huyo alishtakiwa mwezi mmoja baada ya kukamatwa na kufikishwa kortini kwa mwanamke mwingine Bi Faith Wairimu Maina aliyedaiwa aliwapa Sh40,000 wamuue mumewe Bw John Muthee Guama.
Bi Maina alishtua ulimwengu alipokiri kwamba alipanga njama za kumwangamiza mumewe Bw Guama anayeuza matunda ya Macadamia.
Alikiri shtaka lakini akabadilisha nia  baadaye na kukanusha shtaka hilo.
Bi Maina anayetetewa na Bw Swaka aliachiliwa kwa dhamana ya pesa tasilimu Sh1milioni ama awasilishwe mdhamini wa Sh3milioni.
Kabla ya kubadilisha nia na kukana mashtaka Bi Maina alisemekana alikuwa amepanga na wauaji kwamba watamletea nguo za mumewe zikiwa zimelowa damu.
Bi Maina alikana  alipanga njama hiyo katika mtaa wa Zimmerman mnamo Juni 17, 2013.