Afisa Habari Mkuu wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora Germanus Kyafula(kushoto)akieleza kwa vyombo vya habari nchini kuhusu mfumo mpya wa kupokea malalamiko kwa njia ya ujumbe wa simu ya kiganjani katika mkutano uliofanyika katika ukumbi wa Idara ya Habari leo jijini Dar es salaam, kulia ni Mkuu wa Kitengo cha Usimamizi wa Mifumo ya Taarifa Wilfred Warioba.
Baadhi ya waandishi wa habari wakifuatilia kwa makini taarifa inayotolewa na maafisa wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora katika mkutano uliofanyika ukumbi wa Idara ya Habari leo jijini Dar es salaam.
Mkuu wa Kitengo cha Usimamizi wa Mifumo ya Taarifa Wilfred Warioba(katikati) akifafanua jambo kwa waandishi wa habari kuhusu mfumo mpya wa kupokea malalamiko kwa njia ya ujumbe wa simu ya kiganjani kushoto ni Afisa Habari Mkuu wa Tume hiyo Germanus Kyafula na kulia ni Mkurugenzi Msaidizi wa Idara ya Habari.
Mkurugenzi wa Idara ya Haki za Binadamu Francis Nzuki akiwaonesha waandishi wa habari kijitabu chenye sheria namba 7 ya mwaka 2001 iliyounda Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora, katika mkutano uliofanyika ukumbi wa Idara ya Habari leo jijini Dar es salaam kulia ni Kaimu Mkurugenzi Elimu kwa Umma na Mafunzo Alexander Hassan.PICHA ZOTE NA FRANK MVUNGI.
Na Georgina Misama-MAELEZO
Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora imeanzisha mfumo mpya wa kupokea malalamiko na taarifa kuhusu uvunjwaji wa haki za binadamu na ukiukwaji wa misingi ya utawala bora kwa njia ya ujumbe wa simu ya kiganjani.
Hayo yamesemwa na Msemaji wa Tume hiyo Germanus Kyafula wakati akizungumza na waandishi wa Habari leo Jijini Dar es Salaam. "Tume imeamua kuanzisha utaratibu huu mpya, ambapo watanzania watakuwa na fursa ya kuwasilisha malalamiko yao wakati wowote bila ya kuja kwenye ofisi zetu au kutumia barua kwa njia ya posta kama ilivyokuwa awali"alisema Germanus .
Akifafanua utaratibu huo alisema mwananchi atatakiwa kuandika ujumbe mfupi wa simu ya kiganjani kwenda namba 0754 460259 ili kufungua malalamiko pale ambapo ataona haki zake za msingi zimekiukwa au misingi ya utawala bora haijafuatwa.Aidha Germanus alisema utaratibu huu mpya ulianza tarehe 27 Juni na mpaka sasa umeongeza idadi ya malalamiko yanayowasilishwa na wananchi kutoka sehemu mbalimbali ambapo Tume ishapokea malalamiko 127.
Naye Mkurugenzi wa Idara ya haki za Binadamu Francis Nzuki akitoa ufafanuzi alisema Tume itashirikiana na mashirika yasiyo ya kiserikali katika kutoa elimu kwa wananchi kuhusu haki za bunadamu na kutoa vipeperushi ambavyo vina taarifa ya huduma hiyo. Tume imesema ina mkakati wa kusogeza huduma kwa wananchi, lengo ni kuwafikia watanzania wengi iwezekanavyo hasa wananchi wa vijijini.
Tume ya haki za binadamu na utawa bora imesema sambamba na utaraibu huu mpya, bado inaendelea kupoke malalamiko kwa utaratibu wa zamani ambapo wananchi walikuwa wakifika wenyewe kwenye ofisi za Tume na kufungua jalada la malalamiko yao.
0 comments:
Chapisha Maoni