TAIFA STARS, SUDAN ZATOKA SULUHU
Timu
ya Taifa ya Tanzania (Taifa Stars) imetoka sare ya bila kufungana na
Sudan (Nile Crodcodile) katika mechi ya kujipima nguvu iliyochezwa leo
(Juni 2 mwaka huu) kwenye Uwanja wa Addis Ababa nchini Ethiopia.
Mechi
hiyo iliyochezeshwa na mwamuzi Bamlak Tessema wa Ethiopia ilikuwa
sehemu ya maandalizi kwa timu zote ambazo wikiendi ijayo zinacheza mechi
za mchujo za Kombe la Dunia. Wakati Stars itakuwa ugenini nchini
Morocco, Sudan itacheza nyumbani dhidi ya Ghana.
Stars
inayodhaminiwa na Kilimanjaro Premium Lager ilicheza vizuri mechi hiyo,
hasa kipindi cha pili ambapo ilifanikiwa kutengeneza nafasi kadhaa za
kufunga lakini ama washambuliaji walipiga nje au mipira yao kuokolewa na
kipa Ehab Abdelfatahh wa Sudan.
Washambualiji
wa Stars akina Khamis Mcha, Mrisho Ngasa na Amri Kiemba wakiongozwa na
John Bocco walilitia msukosuko mara kwa mara lango la Sudan ambalo
lilikuwa chini ya beki wa kati Nadir Eltayeb ambaye alifanya kazi ya
ziada dakika ya 72 kuokoa mpira uliokuwa ukielekea wavuni.
Stars
katika mechi hiyo iliwakilishwa na Juma Kaseja, Nadir Haroub/Vicent
Barnabas, Shomari Kapombe, Kelvin Yondani, Aggrey Morris, Frank Domayo,
Mrisho Ngasa, Salum Abubakar, John Bocco/Haruni Chanongo, Amri
Kiemba/Khamis Mcha na Simon Msuva/Athuman Idd.
Balozi
wa Tanzania nchini Ethiopia, Joram Biswaro amewataka wachezaji wa Taifa
Stars kuhakikisha wanaipeleka timu hiyo kwenye fainali za Kombe la
Dunia zitakazofanyika mwakani nchini Brazil.
Timu inaondoka kesho alfajiri kwenda Morocco kwa kupitia Cairo, Misri ambapo inatarajia kuwasili Casablanca saa 8 mchana.
Boniface Wambura
Ofisa Habari
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF)
Addis Ababa
+251 919910240
0 comments:
Chapisha Maoni