Searching...
Ijumaa, 7 Juni 2013

SIMBA NA YANGA KUSHIRIKI MICHUANO YA CHALLENGE HUKO DAFUR - SUDANI SASA KUSUBIRI TAMKO LA SERIKALI TFF WANAWA MIKONO.

 
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

Juni 7, 2013
USHIRIKI DARFUR MIKONONI MWA SERIKALI- TENGA


Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Leodegar Tenga amesema kuwa ushiriki wa klabu za Tanzania kwenye mashindano ya Kombe la Kagame yaliyopangwa kufanyika kwenye miji ya Darfur Kaskazini na Gordofan Kusini nchini Sudan unategemea tamko la Serikali ambayo kwa sasa inafanya tathmini ya hali ya usalama.
Tenga, ambaye alikuwa akizungumza na waandishi wa habari kwenye ofisi za TFF leo, alisema tayari TFF na Serikali zimeshafanya mazungumzo, na Serikali imepewa taarifa zote muhimu kuhusu mashindano kwa ujumla, malazi ya klabu za Tanzania, uhakika wa usalama, usafiri wa ndani na mambo mengine muhimu hivyo kwa sasa Serikali inatathmini taarifa hizo kabla ya kutoa tamko.


“Masuala ya usalama yako nje ya uwezo wa CECAFA. Kwa hiyo, kama Serikali itabaini kuwa hali usalama ya huko si nzuri, hatutaziruhusu na kama ikiona hali ni nzuri, itaruhusu,” alisema Tenga.


“Jukumu la CECAFA (Baraza la Vyama vya Mpira wa Miguu vya Nchi za Afrika Mashariki na Kati) ni kuandaa mashindano na kupata uhakika wa usalama kutoka nchi mwenyeji.

“Kama tukipata uhakika huo wa usalama, mashindano yanafanyika. Lakini nchi moja moja zinayo haki ya kuhoji usalama kwa kuwa ni wajibu wa Serikali hizo kujali maisha ya wananchi wake.”


Tenga alisema kuwa mashindano hayo yalikuwa yafanyike Ethiopia, lakini katika dakika za mwisho nchi hiyo iliomba isiandae mashindano hayo hadi mwakani na ndipo Sudan ilipojitokeza kuokoa mashindano hayo.


Alisema wakati wa Mkutano Mkuu wa Shirikisho la Kimataifa la Vyama vya Mpira wa Miguu (FIFA) uliofanyika Mauritius, CECAFA iliitisha mkutano mkuu wa dharura na kupewa taarifa ya maandalizi ya mashindano hayo kutoka uongozi wa Chama cha Mpira wa Miguu cha Sudan na wanachama wakaridhia baada ya kuhakikishiwa usalama.


“Hivyo nchi wanachama wa CECAFA zimeridhia kushiriki baada ya kuhakikishiwa usalama, lakini kwa kuwa Waziri wetu ameonyesha wasiwasi kuhusu usalama wa Darfur, hatuna la kufanya zaidi ya kumsikiliza. Ni kauli ya kiongozi anayeonekana kuwajibika na ni lazima tusubiri tamko la Serikali,” alisema Tenga.


“Lakini napenda kuishukuru Serikali ya Sudan kwa uamuzi huo kwa sababu kuandaa mashindano hayo si kitu kidogo. Tayari Katibu Mkuu wa CECAFA (Nicholas Musonye) ameshakwenda kwenye maeneo hayo na kukaa wiki nzima akikagua viwanja na hoteli zitakazotumika na kuridhika nazo,” alisema.


Alisema watu wasipotoshe tamko la Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe alilolitoa Bungeni kuhusu ushiriki wa timu zetu Darfur.


“Mhe. Membe alisema Serikali itafanya uchunguzi ijihakikishie kuwa hali ya usalama ni nzuri… alisema Serikali haitakubali kuruhusu raia wake kwenda Darfur wakati hali ya usalama si nzuri,” alisema Tenga.


“Kwa maana hiyo, na baada ya TFF kuipa Serikali taarifa zote muhimu kuhusu hali itakavyokuwa wakati wa mashindano, sasa tunasubiri tamko la Serikali. Na hii ni kawaida kabisa kwa kuwa hata hapa tunapoaandaa mashindano, ni lazima kwanza tupata uhakika wa usalama kutoka serikalini ndipo tuziite timu.”


Alifafanua kuwa si jukumu la CECAFA kuamua mashindano yafanyike mji gani na kwamba chama cha nchi mwenyeji ndicho kinachoamua mashindano yafanyike mji gani.


“Sasa kwa suala la Sudan, magavana wa majimbo hayo mawili ya Darfur Kaskazini na Gordofan Kusini waliomba kwa chama chao mashindano hayo yafanyike kwenye miji hiyo na Serikali ya Sudan ikaihakikishia CECAFA usalama,” alisema.

“Sasa ikitokea Serikali yetu ikasema hali si nzuri, hatutaziruhusu timu zetu ziende kwa sababu masuala ya usalama yako nje ya CECAFA.”




0 comments:

Chapisha Maoni

 
Back to top!