Moja
ya barabara za mitaa kata ya Iwawa Makete mjini zikiwa zimelundikwa
vifusi kwa zaidi ya miezi mitatu sasa huku kukiwa na kibao kikionesha
barabara imefungwa ilihali magari yanapita hivyohivyo licha ya maelekezo
ya kibao hicho
Vifusi vikiwa vimelundikwa barabara ya kuelekea hospitali ya wilaya ya Makete.
Hapa inalazimu magari kupita kwenye mifereji
Vifusi vingine hadi vimeyeyuka kutokana na kukaa muda mrefu
Wananchi wa kata ya Iwawa wilayani Makete ambao ni watumiaji
wakubwa wa barabara za mitaa katika kata hiyo, wameiomba halmashauri ya wilaya
ya Makete kusambaza vifusi vilivyopo katika barabara hizo ambavyo vimewekwa
zaidi ya miezi mitatu sasa
Wananchi hao wametoa ombi hilo kufuatia adha wanayoipata
hasa wanapotumia magari kwa kuwa barabara hizo zimekuwa nyembamba hivyo kuleta
usumbufu kwa watumiaji hasa wakati wa magari kupishana
Mmoja wa mwananchi aliyezungumza na ripota wetu Bw. Sipati Mbwilo amesema wanashangaa vifusi hivyo kukaa muda mrefu barabarani bila kusambazwa, jambo linalosababisha usumbufu kwa watumiaji na wakati mwingine kulazimika kuzunguka kupita kwenye barabara nyingine ili kufuata huduma hata kama huduma hiyo ipo jirani
“Unajua braza unaweza kukuta umepata kazi ya kupeleka kuni
ama kwenda kuchukua kuni kwa gari, lakini inakulazimu uzunguke umbali mrefu ili
kukwepa hivi vifusi ambavyo hatujui vitasambazwa lini, ni bora wangeviweka
pindi watakapokuwa tayari kuvisambaza leo mwezi wa tatu vifusi vipo barabarani
mambo gani haya” alisema Mbwilo
Naye dereva wa lori aliyejitaja kwa jina la Kisauti amesema
vifusi hivyo vinawapa tabu wanaoendesha magari makubwa kutokana na wembamba wa
barabara na wakati mwingine kulazimika kukataa baadhi ya kazi wanazozipata
kutokana na magari yao kushindwa kupita kwenye barabara hizo
Ripota wetu amezungumza na mhandisi wa ujenzi wilaya ya
Makete Mhandisi Samwel Ndoveni ambaye amekiri kuwepo hali hiyo lakini amesema
kero hiyo itaondolewa hivi karibuni kwa kuwa msimu wa mvua uliokuwa ukikwamisha
utekelezaji wa zoezi hilo unamalizika na mkandarasi ataanza kazi mara moja
Amesema kwa mwaka huu mvua zilinyesha kwa wingi na ndiyo
maana zoezi hilo lilishindwa kutekelezeka kwa wakati kama ofisi yake ilivyokuwa
imepanga
“Ni heri lawama za kutokusambaza vifusi zitupate kuliko
tungesambaza vifusi wakati mvua inanyesha, matokeo yake tungetengeneza tope
jingi na barabara zisingepitika huo ungekuwa ni uharibifu wa fedha za serikali”
alisema Mhandisi Ndoveni
0 comments:
Chapisha Maoni