Mnamo
tarehe 23 April, 2013 majira ya saa tisa alasiri, huko wilayani Liwale
mkoani Lindi, kundi la watu wanaodhaniwa kuwa ni wakulima wa Korosho
walijaribu kuzuia gari lililokuwa na malipo ya korosho wakipinga malipo
ya pili ya Korosho na kuanza kufanya vurugu na uhalibifu mkubwa wa mali,
ambapo
mpaka
sasa taarifa za awali zinaonyesha kuwa nyumba kumi na nne (14)
zimechomwa moto, baadhi ya mifugo imejeruhiwa na kuangamizwa na
kufanyika uharibifu wa miundombinu ya barabara.
Kufuatia
tukio hilo, Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini, IGP Said Mwema ametuma timu
maalum ikiongozwa na Kaimu Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai
nchini DCP Issaya Mngulu kwenda kuongeza nguvu mkoani humo kwa
kushirikiana na uongozi wa mkoa katika kuhakikisha kuwa hali ya amani na
utulivu inarejea haraka na wale wote waliohusika kufanya vitendo vya
uhalifu wanakamatwa na kufikishwa mahakamani ili sheria iweze kuchukua
mkondo wake, mpaka sasa jumla ya watuhumiwa kumi na tisa (19)
wamekamatwa kwa mahojiano.
Aidha, Jeshi la Polisi nchini linalaani vikali vitendo hivyo vya wananchi kujichukulia sheria mkononi na badala yake kuwataka wananchi kufuata njia ya kufanya majadiliano pale ambapo kutakuwa na migogoro ya aina yoyote ndani ya jamii. Majadiliano yatasaidia kuepusha madhara yanayojitokeza ikiwemo watu kupoteza maisha, uhalibifu wa mali na misongamano ya wahalifu magerezani.
Wakati
hatua hizo za kisheria zinaendelea kuchukuliwa, Jeshi la Polisi
linawaomba wananchi kuwa watulivu na waendelee kutoa ushirikiano ili
kuweza kuwabaini wahalifu hao wachache wanaochochea vitendo vya vurugu
na kufanya uhalibifu wa mali ili hatiamae waweze kufikishwa kwenye
vyombo vya sheria. Taarifa zaidi juu ya tukio hili zitaendelea kutolewa
na uongozi wa mkoa wa Lindi baada ya tathmini ya uharibifu uliofanyika
kukamilika.
Imetolewa na:-
Advera Senso- SSP
Msemaji wa Jeshi la Polisi (TZ).
0 comments:
Chapisha Maoni