Searching...
Jumatano, 5 Februari 2014

WAUAWA KWA TUHUMA ZA KUZUIA MVUA KUNYESHA WILAYANI MASWA

Watu wawili wa familia moja wameuawa wilayani Maswa mkoani Simiyu, kwa kupigwa na wananchi waliojichukulia sheria mikononi, wakiwatuhumu kuzuia mvua kunyesha hivyo kusababisha ukame kwenye eneo lao.

Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Simiyu, Charles Mkumbo alitaja waliouawa ni Gilya Chile (70) na mjukuu wake, Nyangu Nyambalya (30). Polisi inashikilia watu wanane akiwemo Kamanda wa Sungusungu, Sosoma Masamuda (50), Ligwa Malimi wakituhumiwa kuhusika na mauaji hayo. 

Wengine ni Emanuel Kasmiri (42), Michael Sospeter (18), Toto Emanuel (28), Nyanzobe Ntinga (26) Tabu Zengo (31) na Joyce Kija (30). Baada ya uchunguzi wa polisi kukamilika, watafikishwa mahakamani kujibu mashitaka.

Mauaji hayo yalifanyika usiku wa kuamkia juzi katika kijiji hicho, Kata ya Mwanhonoli wilayani  Maswa. Inadaiwa sungusungu wa kijiji hicho waliitana usiku na kuafikia katika kikao chao kwenda kuwaamsha babu na mjukuu wake  waeleze sababu za kuzuia mvua kunyesha.

''Usiku huo walinzi hao wa jadi waliwakamata watuhumiwa hao waliokuwa wamelala nyumba tofauti wakawahoji kwa nyakati na maeneo tofauti na kuwataka watoe maelezo ya kutosha ya sababu ya wao kuzuia mvua isinyeshe mpaka mazao kuanza kukauka katika mashamba ya wakulima wa kijiji hicho,'' alisema kamanda. 

Inadaiwa sungusungu hawakuridhishwa na maelezo ndipo walianza kuwasulubu kwa kipigo na kuwasababishia mauti kabla ya kuteketeza miili yao. 

Kamanda alisema, uchunguzi wa awali wa polisi umebaini kabla ya vifo vyao, watuhumiwa walikuwa wakitamba kwenye vilabu vya pombe kuwa wanatoka kwenye familia ya kitemi hivyo wana uwezo wa kuleta mvua au kuizuia isinyeshe. 

Kwa mujibu wa kamanda, tambo hizo zilifanyika kipindi ambacho kijiji hicho kilikumbwa na ukame. Inadaiwa watu hao walishauri wananchi wa kijiji hicho wawachangie gunia moja la mahindi au mtama kila kaya walete mvua.

0 comments:

Chapisha Maoni

 
Back to top!