Searching...
Jumatano, 19 Februari 2014

WAETHIOPIA 100 WAKAMATWA MKOANI PWANI

WAHAMIAJI haramu 100 raia wa Ethiopia wanashikiliwa na jeshi la Polisi mkoani Pwani kwa tuhuma ya kukutwa wameingia nchini bila kibali huku wakijua kuwa kufanya hivyo ni makosa kisheria.
Raia hao wamekamatwa ndani ya siku mbili mfululizo katika maeneo tofauti ambapo kati yao Waethiopia 33 wao wametiwa mbaroni Februari 16 huko kijiji cha Mwidu tarafa ya Chalinze wilayani Bagamoyo na 67 wamebambwa februari 18 eneo la Mlandizi Kibaha.
Kaimu Kamanda wa Polisi mkoani Pwani Mrakibu Msaidizi mwandamizi (SSP) Athumani Mwambalaswa amethibitisha kukamatwa wahamiaji hao ambapo amesema wote wamekamatwa majira ya saa nne asubuhi katika maeneo hayo wakati askari polisi wakiwa doria.
Kamanda Mwambalaswa amesema raia 33 waliokamatwa huko kijiji cha Mwidu wao walikutwa wakiwa wamejificha katika msitu wa Magereza wakati askari wakifanya ukaguzi maeneo hayo .
Ameongeza kuwa katika tukio la pili waethiopia 67 nao wamekamatwa wakiwa wamepakiwa kwenye gari T 943 BET aina ya Fusso lililokuwa likiendeshwa na Ezekia Samson (31) huko Vikuruti Kibaha katika barabara kuu ya Bagamoyo –Mlandizi.
Kaimu kamanda huyo amesema kwa sasa wanaendelea kufanya mahojiano na wahamiaji hao na kisha watawakabidhi idara husika ya Uhamiaji kwa hatua zingine za kisheria ikiwemo kufikishwa mahakamani kujibu tuhuma inayowakabili.

0 comments:

Chapisha Maoni

 
Back to top!