MAREHEMU JAMES KISAKA.
Shirikisho
la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) limepokea kwa masikitiko kifo cha
aliyekuwa kocha wa makipa wa Simba, James Kisaka (57) kilichotokea leo
asubuhi (Desemba 25 mwaka huu) katika Hospitali ya Burhani, Dar es
Salaam.
Msiba
huo ni mkubwa katika familia ya mpira wa miguu kwani Kisaka kabla ya
kuwa kocha alikuwa mchezaji katika nafasi ya kipa. Mbali ya Simba, timu
nyingine alizowahi kudakia ni Ndovu ya Arusha, Volcano ya Kenya na Small
Simba ya Zanzibar.
Akiwa
mwanafunzi Shule ya Sekondari Tambaza jijini Dar es Salaam aliwahi
kuchezea timu za Oysterbay Stars, Eleven Stars ya Msasani, Sigara wakati
ikicheza Ligi ya Temeke na Nyota Nyekundu kabla ya kutua Simba.
Pia
alikuwemo kwenye timu ya Taifa ya vijana iliyokwenda Zimbabwe kwenye
sherehe za uhuru wan chi hiyo mwaka 1980. Vilevile alikuwa mmoja wa
wachezaji waliounda kombaini ya Tanzania ya UMISSETA akiwa na akina Said
George, Nico Njohole, George Kulagwa na wengine. Hivyo mchango wake
katika mchezo huu tutaukumbuka daima.
Kwa
mujibu wa kaka wa marehemu, Benny Kisaka, James alikuwa akisumbuliwa na
ugonjwa wa miguu kufa ganzi na matatizo ya kutoona vizuri.
Msiba uko nyumbani kwake Mbezi Mwisho (Kwa Yusuf), na anatarajia kuzikwa nyumbani kwao Kijiji cha Lusanga, Muheza mkoani Tanga.
TFF
tunatoa pole kwa familia ya marehemu Kisaka, klabu ya Simba na Chama
cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Dar es Salaam (DRFA) na kuwataka kuwa na
subira na uvumilivu katika kipindi hiki kigumu cha msiba huo mzito.
Marehemu Kisaka ameacha mjane na watoto wanne. Bwana alitoa, Bwana ametwaa. Jina lake lihimidiwe.
Boniface Wambura Mgoyo
Kaimu Katibu Mkuu
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF)
0 comments:
Chapisha Maoni