Makamu wa Rais wa Marekani, Joe Biden, amesema China na nchi yake lazima
zitanue ushirikiano wa kivitendo wenye kuonesha matokeo huku akikosoa
mfumo wa elimu na utawala wa China.
Biden amewasili China mapema leo, alikopokelewa kwa gwaride la kijeshi,
na kisha moja kwa moja akaelekea ubalozi wa nchi yake jijini Beijing.
Ziara hiyo ya ghafla ubalozini, ilikusudiwa kuunga mkono mpango wa
Marekani kupunguza vikwazo vya Wachina wanaotaka kuingia Marekani.
Biden ameliambia kundi la watu hao, wengi wao vijana, kwamba anatarajia
wakati wa kutembelea kwao Marekani watajifunza kwamba uvumbuzi unakuja
tu pale mtu anapopumua kwa uhuru.
"Nchini Marekani, watoto wanazawadiwa kwa kuupa changamoto mfumo uliopo
na sio kuadhibiwa. Njia pekee ya kukifanya kitu kuwa kipya kabisa, ni
kukivunja kikongwe." Biden aliwaambia vijana hao.
Kauli kama hii inayouokosoa mfumo wa utawala na kielimu wa China iliwahi kuzua mzozo baina ya nchi hizo mbili siku za nyuma.
Wakati Biden alipowaambia wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Pennsylvania mwezi
Mei mwaka huu kwamba huwezi kufikiri tafauti katika taifa ambalo huwezi
kuvuta hewa kwa uhuru, wanafunzi wa Kichina kwenye chuo hicho walisema
wametukanwa na wakataka waombwe radhi.
Biden amewasili China akitokea Japan, ambako mazungumzo yake ya
hapo jana na viongozi wa Japan, yalituwama juu ya hatua ya China
kutangaza eneo la ulinzi wa anga katika eneo linalojumuisha visiwa
vinavyozizaniwa kwenye Bahari ya Kusini. Marekani, Japan na Korea ya
Kusini zinapingana vikali na hatua hiyo.
Aliwaambia viongozi wa Japan hapo jana kwamba Marekani inatiwa wasiwasi
sana na hatua hiyo ya China na kusema kwamba inaongeza hatari za kutokea
kwa ajali, suala ambalo atalizusha leo kwenye mazungumzo yake na Rais
Xi Jinping wa China.
Amekutana na Makamu wa Rais wa China, Li Yuanchao, kwenye jengo la
Ukumbi wa Watu wa China, ambapo alisifia jitihada za Rais Xi katika
kutatua tafauti zilizopo baina ya Marekani na China. Biden atakuwa na
mazungumzo na Rais Xi baadaye jioni ya leo.
Na kabla ya kuondoka hapo kesho, atakuwa na mazungumzo na
wafanyabiashara wa Kimarekani nchini China kwenye chai ya asubuhi na
baadaye kukutana na Waziri Mkuu wa China, Li Keqiang. Baadaye ataelekea
Korea ya Kusini ikiwa ni kituo chake cha mwisho cha ziara hii ya Asia ya
Mbali.
Mwandishi: Mohammed Khelef/AFP/Reuters
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman
0 comments:
Chapisha Maoni