WATU 16 wameuawa mkoani Tanga katika
kipindi cha miezi 10 kuanzia Januari hadi Oktoba kutokana na ama wivu wa
mapenzi au kukamatwa ugoni.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Tanga,
Costantine Massawe alitoa taarifa hiyo hivi karibuni wakati akiwasilisha
taarifa kwa vyombo vya habari kuhusu hali ya ukatili wa kijinsia na
watoto mkoani humo kati ya Januari na Oktoba mwaka huu.
Kwa mujibu wa Kamanda, mauaji hayo ni
sehemu ya matukio 377 ya ukatili wa kijinsia yaliyojitokeza katika
kipindi hicho. Mengine ni makosa 308 ya ubakaji, 46 ya ulawiti, manne ya
kutupa watoto na matatu ya wizi wa watoto.
Alisema kati ya matukio hayo, kesi 138
ndizo zinaendelea kusikilizwa zikiwa katika hatua mbalimbali mahakamani.
Kesi 166 zinaendelea kupelelezwa na polisi, 57 zilifungwa kutokana na
kukosa ushahidi wa kuzipeleka kwa Mwanasheria wa Serikali kwa hatua
zaidi za kisheria , 24 zilipata ushindi na kesi sita zilishindwa.
Kamanda ameshauri iwepo miongozo ya
kitaifa inayounganisha taasisi muhimu zinazojihusisha na harakati za
kupinga vitendo vya ukatili wa kijinsia.
Alisema ukosefu wa miongozo hiyo, unadumaza kasi ya harakati za kupinga vitendo hivyo.
Alisema viashiria vinavyotokana na
kuwepo kwa matukio ya aina mbalimbali ya ukatili vinadhihirisha kwamba
hali ni mbaya mkoani humo na kwamba jitihada za makusudi zinahitajika
kuunganisha nguvu kwa pamoja.
“Takwimu zetu za matukio yaliyoripotiwa
kwenye vituo mbalimbali vya Polisi zinaonesha kuwepo kwa makosa haya
ambayo ki msingi yanaathiri sana ustawi wa afya ya mwili, akili ya
mwathirika pamoja na kuchochea ukiukwaji wa haki za binadamu ndani ya
jamii”, alisema na kuongeza.
Kutokana na hali hiyo alisema ipo haja
Serikali kujitathmini na kuboresha taratibu za kushughulikia matukio
hayo ikiwemo kuunganisha na kuwezesha vyombo vyote vinavyosimamia sheria
ili kurahisisha utekelezaji wa majukumu yake katika mchakato mzima wa
kupambana na ukatili wa kijinsia.

0 comments:
Chapisha Maoni