Searching...
Jumatatu, 7 Oktoba 2013

ZITO KABWE AANZA ZIARA KANDA YA MAGHARIBI,KUWASHA MOTO TABORA,KATAVI NA KIGOMA

Naibu Katibu Mkuu CHADEMA, Naibu Kiongozi wa Upinzani Bungeni na Waziri Kivuli wa Fedha na Uchumi ndugu Zitto Kabwe ameanza ziara ya mikoa ya kanda ya Magharibi ya Katavi, Tabora na Kigoma.
Lengo la ziara ni kukagua uhai wa CHADEMA, kuhamasisha ujenzi wa chama vijijini na kueneza sera za CHADEMA katika kumkomboa Mtanzania.
Naibu Katibu Mkuu atafafanua juhudi za CHADEMA katika kuleta mabadiliko nchini na hasa mabadiliko ya sheria mama ya nchi KATIBA ikiwemo na hoja mbalimbali ambazo CHADEMA inataka ziwemo kwenye Katiba mpya ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ikiwemo Haki ya wananchi kuwa na sauti katika umiliki wa rasilimali, haki ya elimu bora na bure, afya bora na haki ya hifadhi ya jamii.
Naibu Kiongozi wa Upinzani ataelezea juhudi ambazo CHADEMA imefanya Bungeni katika kuisimamia Serikali kupitia hoja mbalimbali za wabunge. Hii ni pamoja na kupambana na ufisadi kwa mfano utoroshaji wa fedha nje na kupambana dhidi ya uporaji wa Ardhi ya wananchi.
Waziri Kivuli wa Fedha atafafanua namna sera mbovu za CCM zinavyoendeleza umasikini wa wananchi wa vijijini na kueleza namna gani sera za CHADEMA zinazolenga kukuza uchumi wa vijijini zitakavyowezesha kutokomeza umasikini kwa kuwekeza vya kutosha katika miundombinu na huduma za kijamii za vijijini.
Mara baada ya kumaliza ziara ya Kanda ya Magharibi na kukamilisha baadhi ya Majukumu ya kibunge na kimataifa katika kupambana na utoroshaji wa Fedha kutoka Afrika, Naibu Kiongozi wa Upinzani Bungeni ataendelea na ziara katika mikoa mingine na hasa kanda za Ziwa na Kusini.
Imetolewa na Ofisi ya Mbunge wa Kigoma Kaskazini
Jumamosi, 5 Oktoba 2013, Dar-es-Salaam

0 comments:

Chapisha Maoni

 
Back to top!