Kufuatia mgomo wa malori unaoendelea waziri wa ujenzi Mh. John
Magufuli amesema hatabadilika kwani anasimamia sheria na anayetaka
kugoma aendelee kugoma lakini asipeleke gari lake barabarani huku chama
cha wamiliki wa mabasi Taboa wakitishia kuanza mgomo Octoba nane mwaka
huu kwa madai kuwa mapendekezo yao ya mabasi kusafiri bila kupita mizani
yamepuuzwa.
Kauli ya waziri imekuja siku mbili baada ya
wamiliki wa malori kuanza mgomo Octoba tano mwaka huu uliosababisha
msongamano mkubwa wa magari katika barabara ya Morogoro ambapo amesema
sheria haibadilishwi kwa barua na kuongeza kuwa anayeona ameonewa aende
mahakamani na kwenda mbali zaidi kwa kudai kuwa baada ya wizara kuajiri
wafanyakazi wapya kwenye vituo vya mizani mianya ya rushwa imefungwa
ndio maana wanaozidisha uzito wameamua kugoma.
Kufuatia kauli hiyo ITV imemtafuta msemaji wa
wamiliki wa malori nchini Bw Elias Lukumai ambaye amesema wataendelea
kuegesha malori yao popote yalipo hadi ufumbuzi utakapopatikana huku
katibu mkuu wa Taboa Bw Severin Ngalo akidai kuwa tayari wameshatoa
tangazo la kusitisha huduma usafiri wa mabasi yaendayo mikoani na nchi
jirani hadi maombi yao yatakaposikilizwa.
Kwa upande wao baadhi ya madereva wa malori
wakizungumza na ITV mbali na kuelekeza lawama kwa serikali juu ya
kutokuwashirikisha wamiliki wa malori wakati wa kurejesha asilimia tano
ya uzito unaozidi wameelezea athari wanazopambana nazo baada ya wenye
malori kugoma.
0 comments:
Chapisha Maoni