Padre Xavery Kazimoto Komba  wa Peramiho Seminari jimbo la Songea, akiwa amegeuza mgongo kwa lengo la kuficha sura yake, wakati Waandishi wa habari wakimpiga picha alipokuwa eneo la Mahakama ya wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma, akisubiri kusomewa mashtaka yake.(Picha na Kassian Nyandindi)
Padre mmoja wa Kanisa Katoliki huko Peramiho Seminari jimbo la Songea mkoani Ruvuma, Xavery Kazimoto Komba ambaye alikamatwa na kuwekwa mahabusu, hatimaye leo amepandishwa kizimbani katika Mahakama ya wilaya ya Mbinga mkoani humo, kwa tuhuma ya kutoa hongo ya shilingi milioni moja kwa Mkuu wa wilaya hiyo Senyi Ngaga, kwa lengo la kumshawishi asichukuliwe hatua kwa makosa aliyofanya ya kuwatapeli baadhi ya wakulima wa kahawa wilayani humo.
Padre huyo anatuhumiwa kufanya utapeli huo kwa kutumia kampuni yake ambayo hujishughulisha na kununua kahawa, inayofahamika kwa jina la Songea network Company Limited ambayo yeye ndiye Mkurugenzi wa kampuni hiyo.
Inadaiwa kuwa Kasisi huyo wa kanisa Katoliki alikamatwa na kuswekwa mahabusu katika Kituo kikuu cha Polisi wilayani humo, mapema.... Julai 19 mwaka huu majira ya mchana, kufuatia kutoa hongo ya fedha hizo kwa kutumia utaratibu wa M – pesa kwenda namba ya simu ya Mkuu wa wilaya hiyo ambazo mahakamani hapo hazikutajwa.
Ilidaiwa Mahakamani hapo na Mwendesha mashtaka wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa(TAKUKURU) mkoani Ruvuma, Bi. Maria Mwakatobe mbele ya Hakimu mkazi mfawidhi wa wilaya ya Mbinga, Geofrey Mhini kuwa Xavery Kazimoto Komba anadaiwa kufanya kosa hilo Mei 20 mwaka huu na Mei 26 mwaka huu katika majira tofauti.
Mwakatobe aliendelea kudai kwamba Padre huyo anatuhumiwa mnamo Mei 20 mwaka huu alituma kiasi cha shilingi 400,000 na Mei 26 mwaka huu alituma tena shilingi 600,000 kwenda namba ya simu ya Mkuu wa wilaya ya Mbinga Senyi Ngaga, akiwa na lengo la kumshawishi mkuu wa wilaya hiyo asimchukulie hatua kufuatia shauri ambalo lilikuwa kisheria katika ofisi yake.
Habari kwa hisani ya demashonews.blogspot.com