Searching...
Jumapili, 9 Juni 2013

WAMACHINGA MWANZA WAPAZA SAUTI ZAO


Wafanyabiashara ndogo ndogo maarufu kama machinga wanaofanya biashara zao nje ya soko kuu jijini Mwanza, wamelalamikia utaratibu wa viongozi wao wanaoutumia kuwapanga katika eneo hilo, kwa kuwa utaratibu huo unakiuka maagizo waliyopewa ya wao kufanyia biashara zao katika eneo hilo.
Wakitoa malalamiko hayo hii leo wakati zoezi la kuwapanga vizuri katika maeneo yao ya biashara, wafanyabiashara hao wamedai kwamba wanazingatia taratibu zote zilizowekwa katika maeneo yote yaliyopo nje ya soko hilo, hivyo wanasikitishwa na adha wanayoipata kutoka kwa viongozi hao.

Wamesema miongoni mwa taratibu ambazo zimewekwa katika maeneo hayo ni mda wa wao kuanza kufanya biashara zao ambao ni kuanzia saa nane hadi saa tatu usiku, utaratibu ambao wamesema wanautekeleza vyema.
Akiwa katika majukumu yake ya kutekeleza majukumu yake ya kuwapanga wafanyabiashara hao, Sumun Juma ambae ni mwenyekiti wa uongozi unaofahamika kama Market Street amesema kwamba zoezi wanalolifanya linazingatia hatua zote za kisheria, ambazo ni kuwaweka wafanyabiashara hao pamoja na watu wote wanaotumia maeneo hayo katika hali ya usalama kwa kuwa bila kufanya hivyo wafanyabiashara hao hupanga bidhaa zao hadi barabarani na hivyo kuhatarisha usalama katika maeneo hilo.
Amesema malalamiko ya wafanyabiashara hao hayana maana yoyote hivyo wanapaswa kuzingatia kanuni na sheria zinazowaongoza bila kushurutishwa lengo likiwa ni kuyaweka maeneo yote katika hali ya usafi na hivyo kuwataka wafanyabiashara hao kuwa watiifu katika kutii zoezi hilo la kuwapanga vizuri ili waweze kufanya biashara zao vizuri.
Zoezi la kuwapanga wafanyabiashara hao limekuja siku chache baada ya Uongozi wa Halmashauri ya Jiji la Mwanza kutangaza rasmi kuanza zoezi la kuwapanga wafanyabiashara ndogo ndogo katika maeneo yaliyoidhinishwa kwa wao kufanyia biashara, Pamoja na jumamosi ya mwanzo ya kila mwezi kuwa siku ya usafi wa Jiji la Mwanza, lengo likiwa ni kuliweka Jiji la Mwanza katika hali ya usafi na mazingira sambamba na usalama wao katika maeneo ya biashara.

0 comments:

Chapisha Maoni

 
Back to top!