Baadhi ya wananchi na wakulima wa Kijiji cha Nguruweni wakiwa katika mkutano maalum uliotishwa na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif wa kukabidhiwa hati za umiliki wa mashamba ya kilimo katika maeneo yao.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif akizungumza na wakulima wa Kijiji cha Nguruweni kabla ya kuwakabidhi hati za umiliki wa mashamba ya kilimo wakulima hao.

Balozi Seif akimpatia Hati Bwana Mohd Ali Pili ya kumiliki eneo la kilimo katika Kijiji cha Nguruweni ambako kuliibuka mgogoro uliosababishwa na kuinbgizwa watu wasiohusika na maeneo hayo kwa kilimo. Picha na Hassan Issa wa – OMPR – ZNZ.
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imewatahadharisha Wakulima wa Viijiji vya Ndunduke, Nguruweni na Dole kuhakikisha kwamba maeneo ya kilimo waliyokabidhiwa na Serikali kwa shughuli za Kilimo wanayatumia kama yalivyopangwa na kukubalika na pande hizo mbili.
Wakulima hao wakaonywa kuwa ye yote atakaeamua maeneo hayo kuyakata viwanja kwa ajili ya kujenga nyumba au kuyauza kwa mtu mwengine aelewe kwamba Serikali italazimika kumnyang’anya mkulima huyo mara moja.
Kauli hiyo imetolewa na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi wakati akikabidhi hati za umiliki wa mashamba ya kilimo kwa ajili ya wakulima 40 kati ya 181 wa Kijiji cha Nguruweni waliokuwa wakiilalamikia Serikali kwa kipindi kirefu kuidhinishiwa mashamba wanayoyatumia ili kuendeleza shughuli zao za Kilimo.
Balozi Seif alisema wapo baadhi ya watu wenye tabia ya kuomba mashamba au eka kwa kisingizio cha kuendeleza kilimo lakini badala yake hujenga tamaa inayowaelekeza kuanza kukata viwanja na kuuzia watu wengine.
“ Nataka nitahadharishe kabisa kwamba Mkulima ye yote atakayediriki kutumia fursa aliyopewa na Serikali ya kuendeleza kilimo kwenye shamba alilokabidhiwa na akaamua kufanya vyengine afahamu kwamba Serikali haitasita kunyang’anya shamba hilo mara moja “. Alitahadharisha Balozi Seif.
0 comments:
Chapisha Maoni