WAYNE ROONEY.
Maisha ya Wayne Rooney ndani ya klabu yake ya Manchester United yanaonekana kufikia ukingoni baada ya kocha wake David Moyes kumtimua mazoezini na kumtaka akafanye mazoezi na timu ya vijana chini ya umri wa miaka 21 ya klabu hiyo.
Rooney ambaye anatolewa macho na klabu ya Chelsea, ameshaweka wazi kwamba anataka kuondoka Old Trafford msimu huu lakini tayari mashetani hao wekundu wamezikataa ofa mbili za Chelsea huku wakisisitiza kwamba mchezaji wao kamwe hauzwi.
Hata hivyo mshambuliaji huyo wa kimataifa wa England anachokilazimishia sasa ni kuruhusiwa kuondoka na kwenda kujiunga na klabu anayoitaka japo Moyes amemlazimisha kwenda kufanya mazoezi na timu ya vijana kitu ambacho haijulikani kama Rooney atakikubali.
Picha ilianza pale Rooney alipowasili kwenye uwanja wa mazoezi wa Manchester United wa Carrington jumanne asubuhi ambapo alitarajiwa kufanya mazoezi na kikosi kamili cha United.
Lakini katika hali iliyoonekana kama utani au maigizo baada ya Rooney kufika uwanjani hapo tayari kwa mazoezi Moyes alimwambia aondoke na kuwataka wafanyakazi wasaidizi wake kwamba wahakikishe kwamba Rooney anafanya mazoezi na timu ya vijana chini ya umri wa miaka 21chini ya uangalizi wa Warren Joyce.
Bado haijafahamika kama Rooney alikubaliana na amri hiyo na maamuzi hayo ya Moyes japo imefahamika kwamba Rooney anahitaji kufanya mazoezi ili kujiweka fiti baada ya kuumia bega ili aweza kujumuishwa kwenye kikosi cha timu ya taifa ya England pale watakapowavaa Scotland wiki ijayo.
Chelsea bado wanajipanga kutuma ofa nyingine ya paundi milioni 40 baada ya ofa yao ya paundi milioni 30 kukataliwa wiki iliyopita.
Monaco na Arsenal wametajwa katika orodha ya timu zinazowania saini ya mshambuliaji huyo japo Monaco wanapewa nafasi kubwa zaidi kutokana na msimamo wa Manchester kwamba hata wakiamua kumuuza Rooney hatauzwa kwenye vilabu pinzani katika kugombea ubingwa wa ligi kuu wa England.
0 comments:
Chapisha Maoni