Tahadhari hiyo imekuja baada ya NIPASHE
Jumapili kufanya uchunguzi wa muda mrefu, ambapo imegundua samaki hao
wanauzwa nyakati hizo kukwepa kugundulika.
Imefahamika kwamba...... licha ya Serikali kuwa na
kampeni ya kusaka watu wanaojihusisha na uvuvi huo, bado hali imekuwa
mbaya katika maeneo ya pwani ya bahari ya Hindi.
Maeneo yanayotajwa kukithiri kwa uvuvi wa
mabomu ni Pwani ya Bagamoyo, Kawe katika Manispaa ya Kinondoni na Buyuni
eneo la Kigamboni, Manispaa ya Temeke.
Baadhi ya wavuvi waliofanikiwa kuzungumza
na gazeti hili kwa masharti ya kutotajwa majina yao kwa usalama,
walisema watu wanaojihusisha na uvuvi haramu wanatumia mbinu nyingi za
kuingiza samaki sokoni.
Walisema watu wengi kutokana na kuanza
kuwabaini samaki wa aina hiyo, wavuvi wanawauza kwenye maeneo ya
mikusanyiko ya watu nyakati za jioni bila ya kugundulika kwa urahisi.
MBINU CHAFU
Mmoja wa wavuvi hao, alisema njia nyingine
iliyobuniwa ni kuwaweka kwenye majokofu ili kuwafanya wawe wagumu kama
wanavyokuwa samaki waliovuliwa kihalali.
"Samaki wa mabomu anakuwa laini kutokana
na kuvunjwavunjwa na mlipuko, pia macho yao yanaonekana mekundu kutokana
na kuvilia damu", alisema na kuongeza "Samaki wadogo wanauzwa kwa
wakaanga samaki pale pale ufukweni."
Alisema, samaki wakubwa wanahifadhiwa kwenye jokofu kwa muda wa siku moja ili kuwagandisha na barafu.
"Ugumu wa barafu inasababisha kutopindika kirahisi, ni vigumu kumgundua kama amevuliwa kwa bomu," aliongeza kusema.
SOKO LA FERI
Katibu Mkuu wa Soko la Kimataifa la samaki
la Feri, Mbaraki Kilima, akizungumzia suala hilo, alisema kwamba
wamefanikiwa kudhibiti samaki hao wasiingie kwenye mzunguko wa ndani ya
soko hilo.
Hata hivyo, alikiri kuna kipindi
wanaingizwa kinyemela, lakini wengi wao wanauzwa nje ya soko hasa
maeneo ya kivuko cha Kigamboni.
"Ni kazi ngumu kuwakabili wahusika kwa
sababu wana vitisho, kilichobaki tunakuwa makini samaki kuingia hapa
kwetu pekee," anasema Kilima.
NI VIGUMU KUWAKAMATA
Baadhi ya wavuvi hao walisema ni vigumu kukamatwa kutokana na kuwa na mtandao mkubwa.
Walisema endapo kunatokea zoezi la kuwakamata, wanapata taarifa mapema, hivyo ni rahisi kwao kukimbia.
"Kuna watu wanashirikiana nao sehemu
mbalimbali, viongozi hata polisi, hata sisi inatuwia vigumu kuwataja
kwani tunaweza kuhatarisha maisha yetu,", alisema mmoja wao.
AFISA UVUVI TEMEKE AZUNGUMZA
Afisa Uvuvi wa Manispaa ya Temeke, Teddy
Chuwa aliakiri kuwepo kwa hali hiyo, ambapo alitoa takwimu ya watu zaidi
ya 50 wamekamatwa na kupelekwa Mahakamani.
Alisema wamekuwa na operesheni maalum za kuwakamata watu hao na kupelekea kupungua kwa matukio ya aina hayo kwa asilimia 70.
Chuwa alifafanua kwamba kuna madhara ya
kula samaki waliovuliwa kwa mabomu japo hayajitokezi kwa haraka, hivyo
alionya watu kutowanunua.
Afisa huyo, alisema katika mazingira ya
bahari, mabomu hayo yanaharibu matumbawe ambayo ni mazalia ya samaki
pamoja na kuharibu ikolojia ya viumbe wanaoishi majini.
TFDA WAZUNGUMZA
Afisa Uhusiano wa Mamlaka ya udhibiti wa
Chakula na Dawa (TFDA) Gaudensia Simwanza, akizungumzia suala hilo
alisema, kwamba bado hajapata taarifa kuingia kwa samaki hao sokoni.
"Sisi tunafanya kazi ya kuangalia samaki
wanaoingia sokoni, lakini sijapata taarifa yoyote kama kuna wa aina
hiyo, ngoja niwasiliane na idara ya chakula halafu nitatoa taarifa,"
alisema Simwanza.
Hata hivyo, alisema kuwa udhibiti wa
samaki hao unafanywa na idara ya uvuvi kwa Halmashauri za jijini Dar es
Salaam, endapo zoezi hilo likiendeshwa kwa umakini samaki hao siyo
rahisi kuingia sokoni na kuuzwa kiholela.
CHANZO: NIPASHE
0 comments:
Chapisha Maoni