RAIS NICOLAS MADURO.
Rais wa Venezuela Nicolas Maduro amesema kuwa ameamua kumpa hifadhi
mfanyakazi wa zamani wa shirika la ujasusi la Marekani Edward Snowden,
ambaye ametuma maombi kwa nchi kadhaa ili kuepuka kukamatwa na Marekani.
Akizungumza kwa njia ya televisheni wakati wa sherehe za kuadhimisha
uhuru wa nchi hiyo, Maduro amesema ameamua kumpa Snowden hifadhi ya
kibinadamu katika nchi yake ili aepuke kuandamwa na Marekani. Snowden
anaaminika kuwa amejificha katika eneo la abiria la uwanja wa ndege wa
kimataifa wa Moscow tangu tarehe 23 mwezi uliopita.
Maduro amesema ameamua kumpa Snowden hifadhi kwa sababu siri aliyofichua imeonesha wazi maovu yanayofanywa na taifa la Marekani.
"Nani ana hatia? huyu kijana mdogo ama serikali ya Marekani ambayo
inatoa mabomu na silaha kwa magaidi ambao ni wapinzani nchini Syria
dhidi ya watu wa Syria na kiongozi halali rais Bashar Al Assad?"
Aliuliza Maduro alipokuwa anawahutubia maafisa wa jeshi waliompigia
makofi baada ya tamko lake hilo.
Edward Snowden aliye na umri wa miaka 30 anatakikana na Marekani kwa
kufichua madai ya mpango wa udokozi wa Marekani dhidi ya washirika wake
wa Ulaya. Hata hivyo kwa sasa haijajulikana wazi iwapo Snowden atakubali
hifadhi hiyo au ni vipi atakavyopokea habari hiyo ya kupewa hifadhi na
Rais wa Venezuela.
Awali Urusi ilionesha wasiwasi wake juu ya kuwepo kwa mfanyakazi wa
zamani wa shirika la ujasusi la Marekani nchini mwake, wakati waziri
wake wa mambo ya kigeni Sergei Lavrov aliposema kwamba bado hawajapokea
ombi la kutaka hifadhi kutoka kwa Snowden na kwamba ni lazima atafute
mahali pa kwenda ili aondoke Urusi. Lavrov amesema kila anapozidi kukaa
nchini humo anahatarisha mahusiano mema kati yao na Marekani.
Awali rais wa Nicaragua Daniel Ortega alisema serikali yake iko
tayari pia kumpa hifadhi Edward Snowden. Wakati huo huo Marekani
imekataa kutoa tamko juu ya hatua ya rais Nicholas Maduro.
Shirika la Wikileaks lilisema Snowden ameendelea kuomba hifadhi kwa
mataifa mengine 6 na kuongeza idadi ya nchi alizoomba hifadhi kufikia
zaidi ya 20.
HABARI NA DW - SWAHILI.
0 comments:
Chapisha Maoni