MKURUGENZI
Mtendaji wa Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP), Usu Mallya amefungua
mafunzo ya Ukatili wa Kijinsia na Haki za Binadamu kwa kundi la
washiriki kutoka mikoa na taasisi anuai za umma na binafsi ili
kuwajengea uwezo juu ya mapambano ya masuala upiganiaji haki kwa jamii.
Akizungumza
na washiriki wa semina hiyo, Bi. Mallya aliwataka washiriki kutumia
nafasi waliopata ipasavyo kwa kuhakikisha wanafuatilia mafunzo vizuri
ili kila mmoja atoke kama malozi wa chachu ya mapambano juu ya vitendo
vyote vya kikatili kwa jamii na masuala ya haki za binadamu.
Aliwaeleza
washiriki kila mmoja kwa nafasi aliyonayo sasa anaweza kuwa chachu ya
mabadiliko endapo atatimiza wajibu wake kwenye eneo alipo. Alisema suala
la ukatili wa kijinsia ni suala mtambuka nchini kwani limeenea karibuni
kila eneo la nchi, hivyo kuna kila sababu ya kuzidisha mapambano dhidi
yake.
"...Kwa
kweli suala la ukatili wa kijinsia ni suala mtambuka kwenye maeneo yote
ya nchi yetu, twakwimu za kitaifa zinatuambia takribani asilimia 40 ya
wanawake wote wamekwisha fanyiwa ukatili wa namna moja ama nyingine, kwa
kila wanawake wawili mmoja ameshafanyiwa ukatili wa kijinsia...wengine
tumepigwa, wengine tumefanyiwa ukatili wa kiuchumi, kisaikolojia...,"
alisema Mallya.
Aidha
Mallya aliongeza kuwa ukatili wa kijinsia kwa sasa katika mfumo wa
utandawazi lipo kila upande bila kujali ni kwa wanawake au wanaume,
kwani kila mmoja anaathirika na suala hilo. Alisema lengo la mafunzo
kama hayo ni kuona mabadiliko katika mfumo juu ya kujali na kuheshimu
haki za makundi yote, yaani haki za watoto, haki za kijamii, haki za
watu wenye ulemavu, haki za wanawake haki za vijana n.k.
Alisema
kuwa nchi nyingi za Bara la Afrika zinapambana na mifumo miwili
mikubwa, ambayo ni mfumo wa kitabaka unaoongeza nafasi kati ya matajiri
na masikini (walio nacho na wasionacho) na mfumo dume ambao nao umekuwa
ukiwakandamiza wanawake katika jamii.
Mafunzo
hayo yanaendeshwa na Chuo cha Mafunzo ya Jinsia (GTI) ambacho
kilianzishwa na TGNP ili kuratibu mafunzo anuai ya jinsia chini ya
mwamvuli wa TGNP. Miongoni mwa washiriki katika semina hiyo ni
wawakilishi kutoka madawati ya jinsia ya Jeshi la Polisi, mahakama,
idara ya ustawi wa jamii, washiriki kutoka asasi za watu wenye ulemavu
na wasio na ulemavu na baadhi ya wajumbe kutoka mikoa kadhaa ya
Tanzania.
0 comments:
Chapisha Maoni