Mkurugenzi wa upelelezi wa Makosa
ya Jinai Nchini DCI Robert Manumba akizungumza na Wakurugenzi wa
Upelelezi wa Makosa ya Jinai katika mafunzo ya kufanya Operesheni za
Pamoja kati ya SARPCCO na EAPCCO.Mafunzo hayo yanafanyika jijini DAR Es
Salaam.
Mkurugenzi wa upelelezi wa Makosa
ya Jinai Nchini DCI Robert Manumba akiwa katika picha ya pamoja na
Wakurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai kutoka Nchi mbalimbali za
Afrika ambao wanashiriki mafunzo ya kufanya Operesheni za Pamoja kati ya
SARPCCO na EAPCCO.Mafunzo hayo yanafanyika jijini DAR Es Salaam.
--
Na Frank Geofray-Jeshi la Polisi.
Wakurugenzi wa Upelelezi wa
makosa ya jinai kutoka nchi 25 barani Afrika wametakiwa kutumia vizuri
mafunzo ya Operesheni za pamoja ili kuweza kukabiliana na uhalifu
ikiwemo vitendo vya ugaidi na uhamiaji haramu vinavyojitokeza katika
nchi za Afrika Mashariki na Kusini mwa Afrika kwa kasi hivi sasa.
Hayo yamesemwa jana na
Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai Nchini DCI Robert Manumba
wakati akizungumza na waandishi wa habari baada ya kufungua Mafunzo kwa
Wakurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai kutoka Umoja wa Wakuu wa
Polisi Kusini mwa Afrika (SARPCCO) Pamoja na Umoja wa Wakuu wa Polisi
Afrika Mashariki (EAPCCO) kuhusu kufanya operesheni za pamoja
kukabiliana na uhalifu unaovuka mipaka.
DCI Manumba amesema uhalifu
unaofanyika hapa nchini na ukanda huu wa Afrika Mashariki ndio huo huo
unaotokea katika nchi nyingine hivyo ushirikiano na kubadilishana
taarifa kutasaidia kutambua na kuweka mikakati thabiti ya kuweza
kudumisha amani na usalama katika bara la Afrika.
“Kwa mfano suala la Wahamiaji
haramu hatuwezi kupambana nalo sisi wenyewe kwa kuwa wanatoka katika
nchi nyingine na hapa wanapita tu kwenda katika nchini nyingine hivyo
lazima tubadilishane taarifa na kuwa na mkakati wa pamoja wa kuwabaini
wanaofanya vitendo hivyo” Alisema Manumba.
Kwa upande wake Mkuu wa Polisi wa Kimataifa INTEPOL kanda ya Afrika Mashariki kutoka Nchini Kenya Bw.Rego Francis amesema
Majeshi ya Polisi yana wajibu wa kutoa elimu ya kutosha kwa wananchi
ili waweze kutoa taarifa za uhalifu mapema kwa vyombo vya usalama ili
ziweze kufanyiwa kazi mapema kabla ya matukio kutokea.
Naye Mkuu wa Kitengo cha Polisi
wa Kimataifa (INTEPOL) Tanzania Kamishna Msaidizi wa Polisi Gustavus
Babile amesema Mafunzo hayo ya siku mbili lengo lake ni kubadilishana
uzoefu na kupeana mbinu na kuweka mikakati ya kufanya operesheni
zitakazoweza kuutokemeza uhalifu.
Babile alisema kupitia mafunzo
hayo wataweza kuandaa Operesheni zenye mafanikio zitakazoweza
kushirikisha nchi nyingi katika kukabiliana na Ugaidi, Madawa ya
kulevya, wahamiaji haramu, wizi wa magari na uhalifu wa aina nyingine
unaotokea hapa Afrika.
Mafunzo hayo yanafanyika baada
ya kumalizika kwa Mkutano wa kumi na nane wa Wakuu wa Polisi kusini mwa
Afrika SARPCCO ambapo katika maazimio yaliyofikiwa ni pamoja na kufanya
operesheni za pamoja baina ya SARPCCO na EAPCCO.
0 comments:
Chapisha Maoni