Searching...
Ijumaa, 4 Oktoba 2013

TAARIFA YA MTIHANI WA TAIFA WA KIDATO CHA PILI, 2013

JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA
WIZARA YA ELIMU NA MAFUNZO YA UFUNDI
TAARIFA KWA UMMA
1.0 Utangulizi
Mtihani wa Taifa wa Kidato cha Pili kwa mwaka 2013 unatarajiwa kufanyika nchini kote kuanzia tarehe 07/10/2013 hadi tarehe 21/10/2013. Idadi ya shule/vituo vilivyosajili watahiniwa mwaka 2013 ni 4,437 ikiwa ni ongezeko la vituo 140 sawa na asilimia 3.3 ikilinganishwa na vituo 4,297 vilivyosajiliwa mwaka 2012.
2.0 Watahiniwa
Jumla ya watahiniwa 531,457 wamejiandikisha kufanya mtihani huu. Kati yao wasichana ni 270,734 (sawa na asilimia 50.9) na wavulana ni 260,723 (sawa na asilimia 49.1). Aidha, watahiniwa waliojiandikisha wanajumuisha makundi mawili yenye 
mahitaji maalum. Makundi hayo ni  watahiniwa wenye uoni hafifu ambao jumla yao ni 89 na wasioona 93. Karatasi za mtihani wa watahiniwa wenye mahitaji maalum zimeandaliwa kwa kuzingatia mahitaji yao kama vile kutumia karatasi za “Braille” kwa wasioona na kuongeza ukubwa wa maandishi kwa wenye uoni hafifu.
3.0 Umuhimu wa Mtihani wa Kidato cha Pili
Mtihani wa Kidato cha Pili kama ilivyo mitihani mingine ya taifa ni muhimu kwa kuwa:
  • Unapima kiwango cha maarifa na ujuzi alioupata mwanafunzi kutokana na mada alizojifunza katika kidato cha Kwanza na cha Pili.
  • Ni sehemu ya tathmini endelevu katika masomo ya elimu ya sekondari.
  • Unawezesha Wizara na wadau wa elimu kuona umahiri wa Wanafunzi katika masomo mbalimbali.
  • Unatoa changamoto zinazosaidia wanafunzi, walimu, wizara na wadau wote wa elimu kutambua mapungufu yaliyopo katika suala zima la ufundishaji na ujifunzaji ili yaweze kufanyiwa marekebisho kwa lengo la kuboresha elimu.
Pamoja na mtihani huu, Wizara inasisitiza wanafunzi kuongeza juhudi na kujituma katika kujifunza,, kuzingatia maadili, kujenga uadilifu katika masomo yao na kujenga utamaduni wa kusoma vitabu.
Aidha, walimu, wazazi na walezi wanaombwa kuendelea kuwasaidia na kuwaandaa vema wanafunzi ili wafanye mtihani katika hali ya utulivu. Vile vile wizara inasisitiza jamii kushiriki kwa ukamilifu katika kukamilisha mahitaji ya wanafunzi na kuweka mazingira ya shule yawe ya rafiki, bora na stahiki ili kufanikisha zoezi zima la upatikanaji wa Elimu Bora.
Pamoja na changamoto mbalimbali nawaasa wanafunzi wa kidato cha pili kwamba hii ndiyo fursa yao kulionyesha taifa kuwa wanaweza, wanasoma na wanaimarika kielimu, maarifa na ujuzi. Ari yenu iwe “kama wengine waliweza; hata sisi tunaweza na tutafaulu” suala la kushindwa lisiwe sehemu ya ari yenu katika mtihani huu.
4.0 Hitimisho
Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi inaagiza Wadau wote wa elimu katika Kanda, Manispaa na Halmashauri za Wilaya pamoja na Wazazi kuhakikisha kuwa wanafunzi wote waliojiandikisha kufanya mtihani wanafanya mtihani bila kukosa na katika hali ya utulivu.
Nawatakia watahiniwa wote wa mtihani wa Kidato cha Pili kila la heri, utulivu na mafanikio katika mtihani wao. Tunawajali na tunawathamini na tutaendelea kuchukua hatua mbalimbali ili mpate elimu, maarifa na ujuzi ili kushiriki vyema na kwa ufanisi katika ujenzi wa taifa letu.
Mwisho kabisa niwapongeze wamiliki wa shule yaani TAMISEMI na TAMONGSCO pamoja na walimu kwa kazi mliyoifanya kuwaandaa wanafunzi hawa na sasa wanakaribia kufanya mtihani wa kidato cha pili. Tuendelee kushirikiana. Tunazitambua changamoto na tutaendelea kuzishughulikia kwa pamoja ili elimu yetu iimarike.
Prof. Sifuni E. Mchome
Katibu Mkuu
Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi

0 comments:

Chapisha Maoni

 
Back to top!