Searching...
Ijumaa, 23 Agosti 2013

HIVI NDIVYO MITAMBO YA UMEME UBUNGO ILIVYOTEKETEA KWA MOTO.

  Askari wa Kikosi cha zimamoto na Uokoaji wakizima moto uliokuwa unawaka katika mitambo ya kuzalisha umeme ya songas, Ubungo jijini Dar es Salaam jana.
Picha na Francis Dande
Mitambo ya kuzalisha umeme ya Songas iliyopo Ubungo jijini dar es Salaam, usiku wa kuamkia jana  imeungua moto kabla ya kudhibitiwa na Kikosi cha Uokoaji na Zimamoto kwa kushirikiana na kikosi cha Kampuni ya Knight Support.
Akizungumzia tukio hilo, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Umeme nchini (Tanesco), Mhandisi Felichesim Mramba, alisema hitilafu hiyo imetokea katika kituo cha 33kv na kusababisha gridi ya taifa inayotumika jijini Dar es Salaam kuzimika, hivyo baadhi ya maeneo umeme ukawa umekatika.
“Tulipata taarifa saa 10 kuwa kuna hitilafu hapa na tukajaribu kuwasiliana na Idara ya Zimamoto kwa simu wakawa hawapatikani mpaka tulipowafuata ofisini kwao. Nashukuru baada ya taarifa walifika kwa wakati na wakafanikiwa kuudhibiti moto,” alisema.
Alisema kuwa kutokana na hitilafu hiyo maeneo mbalimbali ya jiji yaliyokuwa yakipata umeme kupitia kituo hicho yataathirika na kuyataja kuwa ni Kigogo, Mburahati, Magomeni, Tandale na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.
Meneneo mengine ni Changanyikeni, Kimara, Tabata na Riverside na kwamba juhudi zinafanyika kuangalia uwezekano wa maeneo hayo kuunganishwa katika njia nyingine kwa muda.
Aliongeza kuwa bado hawajajua thamani halisi ya hasara iliyopatikana na muda utakaotumika kufanya marekebisho huku akiainisha kuwa ukarabati wa vifaa hivyo unaweza kuchukua wiki moja mpaka mbili kutegemea na aina ya uharibifu.
Baadhi ya mashuhuda waliliambia gazeti hili kuwa moshi uliokuwa ukitoka katika mitambo hiyo ulikuwa mzito na uliwasababishia kushindwa kupumua vizuri.
“Niliwaona kina mama na watoto waliokuwa wanakwenda katika kituo cha mabasi Ubungo wakipata taabu kupumua hadi tukawa tunawasaidia kuwapeleka mbali na eneo la tukio,” alisema Gervas Lutabalize, ofisa wa Chama cha kutetea abiria.
Kamanda wa Kikosi cha Zima Moto na Uokoaji jijini Dar e s Salaam, ACP Jesward Ikonko, alisema walipata taarifa ya tukio saa 11:58 alfajiri na kufika katika tukio saa 12:5 ambapo waliwakuta wafanyakazi wa kikosi cha Knight Support wakiwa wameshaanza kazi ya kuzima moto.

0 comments:

Chapisha Maoni

 
Back to top!