RATIBA YA KLABU BINGWA ULAYA HII HAPA-NI UJERUMANI vs HISPANIA
Miamba ya soka ya nchini Hispania Real Madrid na Barcelona, watashuka dimbani dhidi ya miamba wa Ujerumani, vilabu vya Borussia Dortmund na Bayern Munich, katika mechi za nusu fainali ya kombe la klabu bingwa barani Ulaya zitakazopigwa baadae mwezi huu.
Kwa mujibu wa ratiba ya UEFA iliyowekwa hadharani inaonyesha mechi za mzunguko wa kwanza za nusu fainali zitapigwa kati ya April 23 na 24, huku marejeano yakiwa April 30 na Mei 1, ambapo mechi zote za awali zitapigwa nchini Ujerumani huku marejeano yakipigwa nchini Uhispania.
Zoezi la upangaji wa ratiba hiyo ambalo lilifanyika nchini Ufaransa yalipo makao makuu ya UEFA, lilishuhudia Bayern Munich wakiangushiwa mikononi mwa Barcelona, huku Dortmund wakitupiwa mikononi mwa Real Madrid.
Matokeo ya kura hizi yameibua hisia za aina yake kwa mashabiki wa soka kote duniani, kutokana na ukweli kuwa, mpangilio wa mechi hizo umeonyesha kuwa hatua hiyo ya nusu fainali itakuwa ni sawa na mapambano baina ya mataifa mawili yenye mafanikio kisoka, Ujerumani na Hispania.
Mechi ya fainali ya michuano hiyo itapigwa katika dimba la Wembley nchini Uingereza, mei 25, huku mshindi baina ya Dortmund na Madrid, akitarajiwa kuwa ndio atakayetambulika kama mwenyeji wa fainali hiyo.
0 comments:
Chapisha Maoni